Mabalozi, Mashirika ya Kimataifa wamemmwagia sifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi uliotukuka na usimamizi mzuri wa masuala ya kijamii, kuimarisha demokrasia na mambo mengine kadha wa kadha, na wamempongeza pia Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kumsaidia Mhe. Rais kusimamia vizuri Sekta ya uchumi na fedha.
Wametoa sifa na pongezi hizo wakati walipokutana Ujumbe wa Serikali kwa muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati wa Ngazi ya Juu kati ya Serikali na Washirika wa maendeleo kwa Mwaka 2024 katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa Serikali, Mkutano huo umewashirikisha Mawaziri; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Pindi Chana, Waziri wa Mifugo, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Kazi, Uchumi na Uwekezaji – Zanzibar, Mhe. Sharifu Ali Sharifu (Mb), Naibu Waziri wa Utamaduni na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mb), Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju, na Wakuu wa Idara.
Kwa upande wa Washirika wa Maendeleo, wao wameongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Mhe. Zlatan Milišić, pamoja na Balozi wa Uingereza nchini ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo, Mhe. David Concar.
Mkutano huo wenye kaulimbiu,”Kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; Kuongeza Kasi ya Uchumi Himilivu na Maendeleo Jumuishi katika Nyakati Zisizotabirika”, umehudhuriwa na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kutoka nchi Washirika wa Maendeleo, pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.