Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bi. Katsura Miyakazi , jijini Dar es Salaam ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya namna kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kimaendeleo kati ya Tanzania na Japan kupitia JICA.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Chriastian Omolo na Mkurugenzi Mkazi wa JICA Bw. Hitoshi Ara, Mhe. Dkt.Nchemba aliishukuru Japan kwa kuchangia maendeleo ya nchi kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika sekta za nishati, afya, kilimo, elimu na miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ambapo alisema Japan kupitia JICA, imeipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1, misaada ya fedha yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.2 na misaada ya kiufundi yenye thaman ya dola za Marekani bilioni 0.9, pamoja na kuwapatia mafunzo mbalimbali ya kitaalam zaidi ya wataalam 22,000 nchini Japan.