Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameiambia Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali ya Tanzania imeendelea kutenga na kuongeza bajeti kila mwaka ya kujenga miundombinu ya uzalishaji nishati likiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 za umeme pamoja na njia yake ya kusambaza umeme, uliogharimu shilingi za Tanzania trilioni 6.6 na dola za Marekani milioni 133.7, kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema hayo wakati akitoa neno wakati wa uwasilishaji wa Mpango Mahsusi wa Serikali ya Tanzania wa Nishati (Compact) wa kuboresha masuala ya Nishati, uliofanyika kando ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi na Serikali, unaofanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam (27 na 28 Januari, 2025), na kusisitiza kuwa Nchi imejipanga kuhakikisha kuwa inafikia lengo la uunganishaji umeme kwa asilimia 75 na kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa umeme lakini pia kufikisha asilimia 75 ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
Mgeni Rasmi katika uwasilishaji wa Mpango huo (Compact), alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na kuhudhuriwa na Viongozi wakuu wa Taasisi za Fedha Duniani akiwemo Bw. Ajay Banga, Rais wa Benki ya Dunia na Dkt. Akinwumi Adesina, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).