Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara na Maendeleo (Trade and Development Bank Group-TDB), Bw. Admassu Tadesse, Kando ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi na Serikali, unaofikia kilele leo (28.01.2025), katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (JNICC), Jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, Mhe. Dkt. Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kipande cha 2 kinachoanzia Morogoro hadi Dodoma, ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Ameiomba Benki hiyo kushiriki pia katika ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kwa kipande (Lot 6, kuanzia Tabora hadi Kigoma na kipande cha 7, ninachoanzia Uvinza hadi Msongati, ambavyo utafutaji fedha wake unaratibiwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), kwa niaba ya Serikali.

Kwa upande wake, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara na Maendeleo (Trade and Development Bank Group-TDB), Bw. Admassu Tadesse, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyopiga kimaendeleo na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa fedha za ujenzi na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam (ujenzi wa gati namba 8 hadi 11 na kuahidi kuwa iko tayari pia kutoa fedha za ujenzi wa SGR kwa kipande cha 6 na cha 7.

Kikao hicho kiliwashirikisha pia, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Naibu wake, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kamishna Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha Bw. Rished Bade, Kamishna wa Idara ya Madeni Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na TDB.

Share Story