Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameshuhudia utiwani saini wa Mikataba ya Ujenzi wa Reli wa Kipande cha Reli namba 7 na 8, kuanzia Uvinza (Tanzania) hadi Msongati (Burundi) kati ya Tanzania, Burundi na Kampuni za ukandarasi za CREGC na CREDC za nchini China, utakaogharimu dola za Marekani bilioni 2.134 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 5.38, tukio lililofanyika Stesheni Kuu ya Shirika la Reli Tanzania-TRC, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa fedha za kukamilisha ujenzi wa mradi huo zipo na zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na kutoa wito kwa Taasisi nyingine za Fedha za Kimataifa kuiga mfano wa Benki hiyo kwa kutoa fedha zitakazo chagiza maendeleo ya nchi za Afrika badala ya kung’ang’ania kutoa fedha za kugharamia semina na kujengeana uwezo, kula chapati na maandazi, mambo ambayo amesema hayana tija kubwa ya kuwakwamua Wananchi kiuchumi.