Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametembelea Kituo cha Pamoja cha Forodha-Tunduma, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Zambia, mkoani Songwe, na kujionea huduma za kiforodha zilizokuwa zikitolewa katika Kituo hicho, ambapo aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusaidia kuboresha miundombinu ikiwemo vitendea kazi vinavyohitajika ili huduma ziendelee kutolewa kwa ufanisi katika Kituo hicho.
Dkt. Nchemba alipita Kituoni hapo akielekea kushiriki tukio la utiaji saini wa kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tunduma-Vwawa – Mlowo, kati ya Serikali kupitia Wizara ya Maji na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), lililofanyika katika Viwanja vya Uwanjani mjini Tunduma, utakaowanufaisha zaidi ya wakazi 219,000 wa miji ya Tunduma, Vwawa na Mlowo, Mkoani Songwe, tarehe 20 Machi 2025.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba, aliambatana na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, Mkuu wa Mkoa Songwe. Mhe. Daniel Chongolo, Wakuu wa Wilaya za Momba na Songwe na Viongozi wengine waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.