Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), usiku wa leo 19 Machi, 2025, amewasili Jijini Mbeya, kwa ajili ya kuwa Mgeni Rasmi katika tukio la utiwaji saini wa makubaliano ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tunduma hadi Vwawa, litakalofanyikat katika Viwanja vya Mwakakati-Tunduma mkoani Songwe, kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi, tarehe 20 Machi, 2025, mradi unaotarajiwa kuwanufaisha maelfu ya wakazi walioko katika eneo la mradi.
Akiwa na Mwenyeji wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, wakati wa futari ya jioni, jijini Mbeya, Dkt. Nchemba, alimpongeza Mhe. Aweso kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Miradi ya Maji nchini na kwamba anamheshimisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu huduma ya maji imewafikia wananchi wengi kupitia usimamizi wake mahiri, na kwamba Wizara yake itaendelea kutimiza maelekezo ya Mhe Rais Dkt. Samia, kuhakikisha kuwa sekta muhimu ya maji inapatiwa fedha za kutosha ili huduma hiyo iwafikie wananchi wengi kama ilivyokusudiwa.