Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa dhamira yake ya dhati ya kuwaondolea adha ya maji, wakazi wa Tunduma, Vwawa na Momba. Kwa kutoa fedha za ndani, kiasi cha sh. bilioni 120, ili kutekeleza mradi wa Maji wa Tunduma-Vwawa, katika Mkoa wake.
Mhe. Chongolo alitoa shukrani hizo Ofisini kwake, wakati akiagana na Mhe. Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso waliofika Mkoani Songwe, eneo la Tunduma, kushuhudia utiwaji saini wa Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Tunduma,- Vwawa, Kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Eng. Mwajuma Waziri, kwa niaba ya Serikali na Meneja Mradi wa Kampuni ya Ukandarasi ya China (China Civil Engineering Construction Corporation-CCECC), Bw. Ning Yunfeng, utakaogharimu shilingi bilioni 119.9 za Tanzania, kutoka chanzo cha maji ya Mto Momba, ulioko Wilayani Momba, mkoani Songwe.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa chanzo cha maji (Intake) chenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 21.5, ujenzi wa Kituo cha kuchakata na kutibu maji chenye uwezo wa kuzalisha lita 20m kwa siku, ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusafirisha maji yenye kipenyo cha 100mm yenye urefu wa kilometa 96, ujenzi wa matenki ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi ujazo wa lita 5m litakalojengwa katika Mtaa wa Uwanjani/Uhuru, Hakmashauri ya Mji-Tunduma, tenki la lita 3m litakalojengwa katika Kijiji cha Ikana na tenki lenye ujazo wa lita 2m litakalojengwa katika Kijiji cha Nkangamo, Ununuzi wa pampu, Ujenzi wa Ofisi na Vitendeakazi vingine.
Akijibu Shukrani hizo Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliahidi kumfikishia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, salaam hizo na kuongeza kuwa dhamira ya Mhe. Rais ni kuhakikisha kuwa huduma ya maji inawafikia Wananchi wa vijijini kwa asilimia 85 na wale wa Mijini asilimia 95 ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2025, ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM, na wajubu wake Kama Waziri wa Fedha ni kuhakikisha fedha zote zinapatikana na zinatoka kwa wakati kadri miradi inavyotekelezwa kwa kuwa maji ni maisha ya wananchi.