Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa kawaida wa Magavana wa Eneo la Afrika Mashariki la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliofanyika katika Hoteli ya Tiama, Jijini Abidjan nchini Côte d’Ivoire, ambao ni mkutano wa kisheria unaowashirikisha Magavana, Magavana Mbadala, Wawakilishi wa Muda, pamoja na wajumbe maalum (kawaida wajumbe wawili) kutoka kila nchi za Afrika Mashariki, Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Eneo husika.
Eneo la Afrika Mashariki ndani ya Benki ya Maendeleo ya Afrika linajumuisha nchi tisa (9), ambazo ni: Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Eritrea, na Shelisheli.
Kwa sasa, Eneo hili linawakilishwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Jonathan Nzayikorera kutoka nchini Rwanda. Mwenyekiti wa Eneo hilo aliyemaliza muda wake wa miaka mitatu ni Mhe. Dkt. Uzziel Ndagijimana, ambaye pia ni Gavana (Waziri wa Fedha) wa Rwanda.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Gavana Mbadala (Alternating Governor) wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha ambaye pia kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji Mbadala wa AfDB, Bw. Rished Bade.