
_▪️Aagiza viongozi kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati_*
_▪️Apiga marufuku kushikiliwa kwa vitendea kazi vya wananchi kwa makosa madogo_*
_▪️Asema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya, elimu na miundombinu_*
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi wa wananchi.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumamosi, Mei 23, 2026 alipozungumza na wananchi wa Manispaa ya Iringa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kichangani mkoani Iringa.
Amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.
“Mheshimiwa Rais ameendelea kuthibitisha kuwa ni Rais wa matokeo. Miradi mingi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa na wananchi wanaendelea kushuhudia maboresho makubwa katika sekta mbalimbali,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na miradi ya kimkakati ili kuimarisha shughuli za uchumi na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini.
“Tunataka kuona miradi yote inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa umma kuhakikisha wanasikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati pamoja na kuondoa urasimu unaochelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Watu wanahitaji kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto zao kwa wakati. Hili si jambo la ziada bali ni wajibu wa viongozi,” amesema.
Pia amepiga marufuku tabia ya kukamata au kushikilia vitendea kazi vya wananchi kama bodaboda, bajaji, magari, baiskeli na bidhaa za wafanyabiashara kwa makosa madogo yasiyo ya jinai kubwa huku akisisitiza kuwa Serikali haitaki kuona wananchi wakidhulumiwa wanapokuwa wakitafuta riziki zao.
“Tusishikilie vitendea kazi vya wananchi wanaotafuta riziki halali isipokuwa pale yanapohusika makosa makubwa ya jinai,” amesema.
Aidha, amezitaka taasisi zinazohusika na huduma za afya kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya sambamba na kusimamia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
“Fedha za dawa lazima ziwanufaishe wananchi. Haiwezekani fedha zitolewe halafu wananchi wakaendelea kuambiwa hakuna dawa hospitalini,” amesema.
Dkt. Mwigulu pia ameagiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyochelewa au kusuasua ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa kwa wakati.
“Miradi inayochelewa inawakosesha wananchi huduma muhimu. Lazima viongozi wasimamie utekelezaji kwa karibu ili thamani ya fedha ionekane,” amesema.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta za elimu, afya na miundombinu katika Manispaa ya Iringa kupitia utoaji wa fedha za maendeleo na ajira kwa watumishi wa sekta mbalimbali.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika Manispaa ya Iringa ambapo madarasa 246 yamejengwa pamoja na shule mpya tano za msingi na sekondari huku zaidi ya shilingi bilioni 10 zikitolewa kugharamia utekelezaji wa elimu bila ada.
Aidha, amesema Serikali imeajiri walimu zaidi ya 139 katika shule za msingi na sekondari ili kuimarisha utoaji wa huduma za elimu na kupunguza uhaba wa walimu katika Manispaa hiyo.
Kwa upande wa afya, Dkt. Dugange amesema Serikali imejenga hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa pamoja na vituo vya afya vinne na zahanati mbili huku watumishi wa afya zaidi ya 157 wakiajiriwa kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 5.7 zimeelekezwa katika ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika vituo vya kutolea huduma.
Aidha, amesema Manispaa ya Iringa ni miongoni mwa halmashauri 45 nchini zinazotekeleza mradi wa uboreshaji wa miji wa TACTIC ambapo zaidi ya shilingi bilioni 20 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya mjini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuielekezea Manispaa ya Iringa zaidi ya shilingi bilioni 634 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi katika sekta za barabara, afya, elimu, maji, umeme pamoja na miradi mingine ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi na kukuza shughuli za kiuchumi katika Manispaa ya Iringa.