aee9c64f-468e-4849-8925-c2b07af80747Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda na kuendeleza urithi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii katika Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Amesema hayo leo (Ijumaa, Julai 3, 2026) alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge, wilayani Butiama, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
“Serikali itaendelea kuipa kipaumbele Butiama na kuboresha miundombinu yake ili kulinda na kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa,” alisema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu aliagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini ya haraka ya barabara za ndani ya Butiama na kuwasilisha makadirio ya fedha ndani ya mwezi mmoja ili utekelezaji uanze kwa awamu kuanzia mwaka huu wa fedha. Alisema barabara hizo ni pamoja na zinazoelekea maeneo ya kihistoria, ikiwemo barabara inayokwenda shambani kwa Baba wa Taifa.