Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kuimarisha malezi ya watoto na vijana, kulinda amani, kuheshimu tofauti na kutimiza wajibu wao kwa taifa, akisisitiza kuwa haki na wajibu haviwezi kutenganishwa.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 25, 2026, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Baraza la Maulid la Kitaifa lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha salamu za Rais, Waziri Mkuu amesema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari, kujifunza na kuyaishi kwa vitendo maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), yakiwemo wema, huruma, upendo na kusaidiana, huku akiwataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika masuala ya maendeleo na malezi, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi, jamii na viongozi wa dini kuongeza uangalizi kwa watoto na vijana ili kuwalinda dhidi ya mmomonyoko wa maadili na athari za matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii. Amesema pamoja na juhudi zilizofanyika kwa miaka mingi katika kuimarisha malezi na ulinzi wa mtoto wa kike, mazingira ya sasa yanahitaji pia kuimarishwa kwa malezi na ulinzi wa mtoto wa kiume.

“Kwa mazingira ya sasa, naweza kudiriki hata kusema kwamba kwa mazingira ya sasa, mtoto wa kiume yuko kwenye mazingira ya hatari zaidi. Kwa hiyo, tuongeze malezi bila kubagua kwamba tumlee zaidi yupi. Wote sasa hivi watoto wako katika mazingira ya hatari.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kuendelea kuwepo kwa utawala bora, amani, usalama na utulivu, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda haki za wengine na kutunza amani ya nchi.

“Na ili tufike hapo, tuendelee kumuombea Rais wetu na tuendelee kuiombea nchi yetu ili tuendelee kuwa na amani na tuendelee kuwa na uimara kama ambavyo taifa letu limeshuhudia kwa kipindi kirefu.”

Kuhusu amani na utulivu, Waziri Mkuu amesema Tanzania inaendelea kuheshimu haki na uhuru wa wananchi, ikiwemo uhuru wa kuabudu na kushiriki katika masuala ya kisiasa, lakini akasisitiza kuwa uhuru huo lazima uende sambamba na kutimiza wajibu na kuheshimu haki za wengine.

“Haki na wajibu inaenda pamoja kwamba unapotaka kupokea kwa mikono miwili haki unayostahili, haki yako hiyo isivunje haki ya wengine. Na hapo ndipo ambapo Katiba yetu imeweka wajibu.”

Ametoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kujenga utamaduni wa kuheshimu tofauti na kuepuka lugha za chuki na uchochezi, akisisitiza kuwa migogoro ya ndani ya jamii na kuvuruga amani ya Taifa havina mshindi.

“Migogoro ya sisi kwa sisi ya wenyewe kwa wenyewe ni migogoro isiyo na mshindi. Kuvunja amani katika taifa hapana mshindi. Hapana mshindi. Hakuna anayeshinda. Kuvuruga taifa hamna mshindi. Hakuna anayeshinda.”

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeiry bin Ally, amewataka viongozi waliochaguliwa katika ngazi mbalimbali za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, kwa kuzingatia mafundisho ya dini pamoja na miongozo na taratibu za taasisi, akiwataka kusimamia haki, maadili na kutoa mwongozo sahihi kwa jamii.

“Kinachotakiwa kwenu nyinyi ni kufanya kazi. Sio hadithi na maneno, ni kufanya kazi kama ambavyo Mungu ametuambia hapa. Fanyeni kazi. Na fanyeni kazi kwa kusimamia haki na maadili na kutoa mwongozo katika jamii ili jamii ipate kutengenea.”

Mufti pia amesisitiza umuhimu wa Waislamu kuendelea kuishi kwa amani, upendo na kusaidiana, huku akihimiza kuimarishwa kwa malezi ya watoto na vijana ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya ukatili.

“Muislamu wa kweli ni yule ambaye watu wako salama kutokana na ulimi wake na mkono wake, na muumini wa kweli ni yule watu wanaomwamini kwa damu zao na mali zao.”

Waziri Mkuu amewapongeza Waislamu wote kwa Maadhimisho ya Maulid na kuwatakia heri, baraka na fanaka, huku akisisitiza kuwa Watanzania wa dini mbalimbali wanapaswa kuendelea kuishi kwa upendo, kuheshimiana na kuilinda amani na mshikamano wa taifa.

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *