
Malipo ya takribani shilingi bilioni 3.8 yaanza
Ununuzi wa pamba kuwa huru msimu unaokuja
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeanza kulipa takribani shilingi bilioni 3.8 kwa wafugaji ambao mifugo yao ilitaifishwa lakini baadaye wakashinda kesi mahakamani.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Novemba 7, 2026), wakati akizungumza na wananchi katika Viwanja vya Polisi Mwandoya, Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
Dkt. Mwigulu amesema malipo hayo yanafuatia maelekezo aliyoyatoa kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu madai ya wafugaji walioshinda kesi zao.
Amewatoa hofu wananchi wenye madai hayo ambao tayari wamewasilisha taarifa zao kwa mamlaka zinazohusika, akiwahakikishia kuwa watalipwa.
“Hamtarejeshewa ng’ombe wenu kama wale walishakufa, lakini mtalipwa thamani ya ng’ombe wenu,” amesema.
Kuhusu pamba, Waziri Mkuu amesema ununuzi wa zao hilo utakuwa huru kuanzia msimu unaokuja, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Wizara ya Kilimo na wadau.
Ameitaka Wizara kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo, kuondoa vikwazo vya ununuzi na kuhakikisha mahitaji ya uzalishaji yanaendelea kupatikana ili kuinua zao hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto shule wanapofikia umri unaostahili, badala ya kuwabakiza katika shughuli za ufugaji.
Akieleza uzoefu wake, amesema jitihada za mwalimu wake za kumshawishi mzazi wake kumrudisha shule zilimsaidia kuendelea na masomo baada ya kwenda kuchunga mifugo.
“Hao hao walio makini tuwapeleke shule. Wakifanikiwa ndiyo wewe mzazi umefanikiwa,” amesema.
Kwa upande wa afya, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa wagonjwa wanaohitaji kupelekwa hospitali za rufaa hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta ya ambulansi za Serikali.
Amehoji pia sababu za wagonjwa kuendelea kuelekezwa kununua dawa nje ya vituo vya Serikali wakati taarifa zinaonesha utoshelevu mkubwa wa dawa, na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokwamisha huduma.
Kuhusu miundombinu, ameelekeza upembuzi yakinifu wa barabara inayounganisha Bariadi, Itilima, Mwandoya na Meatu kuelekea Singida ukamilike mwaka huu wa fedha, ili iingizwe katika bajeti ya mwaka ujao na utekelezaji wake uanze.
Vilevile, ameelekeza wananchi katika maeneo ambayo bado yana mazingira ya vijijini kuunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000, bila kupandishiwa gharama kwa sababu maeneo hayo yamepewa hadhi ya miji midogo.