Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), leo ameongoza kwa vitendo katika kutekeleza haki yake ya msingi ya kidemokrasia kwa kuboresha taarifa zake za Mpiga Kura katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Misigiri, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.
Uboreshaji huu ni sehemu ya Awamu ya Pili ya zoezi la kitaifa la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali, linaloendelea kote nchini kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2025, Tanzania Bara na Zanzibar. Vituo vyote vinapokea wananchi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kila siku.
Mhe. Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kutumia haki na wajibu huu wa kikatiba kwa kujitokeza kuboresha taarifa zao, kuhakiki usahihi wa taarifa, na kuhakikisha kuwa wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu ujao. Amesema: “Uchaguzi ni haki, ni wajibu, na ni chombo cha kulinda amani, maendeleo na usalama wa Taifa letu. Tujitokeze wote.”
Wananchi wote wanaohitaji kuboresha taarifa zao, kujiandikisha kwa mara ya kwanza au kuthibitisha majina yao katika daftari, wanakumbushwa kujitokeza kwa wakati kwenye vituo vyao.
