WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali nchini wametoa wito kwa wadau wa siasa kuacha kumhusisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, na mjadala wa urais wa mwaka 2030, wakisisitiza kuwa kwa sasa anapaswa kupewa nafasi ya kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia Watanzania.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema taarifa zilizochapishwa na gazeti moja hivi karibuni zina lengo la kumdhoofisha kisiasa kiongozi huyo kwasababu hakuwahi kutamka mahali kokote anataka urais huo, hali ambayo wanaona si sahihi ikizingatiwa mchango wake mkubwa katika kushughulikia changamoto za wananchi wa kawaida.

Kwa mujibu wa maoni yao, Dkt. Nchemba amejikita zaidi katika kushughulikia kero za msingi zinazowagusa wananchi moja kwa moja, badala ya kujikita katika siasa za urithi wa madaraka.

“Tunachohitaji sisi ni huduma bora na utatuzi wa changamoto zetu. Waziri Mkuu amekuwa akisikiliza wananchi na kuchukua hatua. Haya mambo ya kumuingiza kwenye siasa za 2030 hayana tija kwa sasa,” alisema mkazi wa Dodoma, ambaye alijitambulisha kwa jina la Joseph Mlay.

Wananchi walitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Waziri Mkuu katika kutatua kero mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushughulikia migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo, kusimamia uboreshaji wa huduma za afya katika hospitali za umma, pamoja na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maji vijijini na mijini.

Aidha, wamepongeza juhudi zake katika kufuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, hali iliyosaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika maeneo mengi ya nchi.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Bi. Rehema Msuya, alisema kuwa kiongozi huyo amekuwa mstari wa mbele kusikiliza kero za wananchi kupitia ziara zake za kikazi.

“Amekuwa akifika hadi maeneo ya chini kabisa, kusikiliza wananchi na kutoa maelekezo ya haraka. Hii imesaidia kupunguza malalamiko mengi ambayo yalikuwa yakipuuzwa hapo awali,” alisema.

Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara wadogo walieleza kuridhishwa na hatua za serikali chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu usio wa lazima na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Mkazi wa Mbeya, Bw. Godfrey Mwakalinga, alisema: “Tunaona mabadiliko kwenye utendaji wa baadhi ya taasisi za umma. Kuna uwajibikaji umeongezeka, na hii inatupa matumaini kwamba mambo yanaenda kuboreka zaidi.”

Hata hivyo, wananchi hao walisisitiza kuwa mjadala wa urais wa mwaka 2030 ni wa mapema na unaweza kupotosha mwelekeo wa viongozi waliopo madarakani, hivyo kuathiri utekelezaji wa majukumu yao ya sasa.

“Ni vyema viongozi wakaachwa wafanye kazi walizopewa kwa sasa. Mambo ya uchaguzi bado yapo mbali. Tusiwachanganye,” alisema mkazi wa Arusha, Bw. Elias Lema.

Kwa ujumla, wananchi hao wameeleza imani yao kwa Waziri Mkuu, wakiamini kuwa endapo ataendelea kupewa ushirikiano na kuondolewa kwenye mijadala ya kisiasa isiyo na tija kwa sasa, ataweza kuleta mabadiliko chanya zaidi katika maisha ya Watanzania.

Wametoa wito kwa vyombo vya habari na wadau wengine wa maendeleo kuzingatia uzalendo na kuandika habari zinazojenga umoja na kuhamasisha maendeleo badala ya kuibua mijadala inayoweza kuvuruga utendaji wa viongozi waliopo madarakani.

#KaziNaUtuTunasongaMbele

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *