_▪️Dkt. Mwigulu asisitiza matumizi sahihi ya rasilimali ili kujenga uchumi wa Afrika_

_▪️Rais Macron atangaza uwekezaji wa dola bilioni 27 Barani Afrika_
 
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Mei 11, 2026 ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward: Africa–France Partnership for Innovation and Growth Summit) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya.
 
Mkutano huo umewakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, teknolojia, nishati, afya, Akili Unde (AI), kilimo, uchumi wa buluu pamoja na viwanda.
 
Akizungumza baada ya mkutano huo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mkutano huo umekuwa wa manufaa kwa Bara la Afrika na Ufaransa kwa pamoja kwani majadiliano yamegusa namna ya kuzifanya pande hizo mbili ziweze kunufaika na ushirikiano huo.
 
Amesema rasilimali zinazopatikana barani Afrika zinatosheleza ikiwa zitatumika vizuri katika kujenga uchumi wa Afrika.
 
“Lengo kubwa la jitihada hizi ni kupambana na umasikini lakini pia na kutengeneza ajira kwa makundi makubwa ikiwemo la vijana pamoja na wanawake,” amesema.
 
Aidha, Waziri Mkuu amesema maeneo mengi yaliyojadiliwa ni maeneo ambayo yamepewa umuhimu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
 
“Nguzo zote zilizoongelewa kwenye dira lakini pia na maeneo ya kipaumbele yameguswa katika mijadala ya leo,” amesema.
 
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto, alizitaka nchi za Afrika kutafakari upya mifumo ya kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali za ndani, uwekezaji pamoja na ushirikiano wa kikanda ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya muda mrefu.
 
Aidha, Rais Ruto amesema ni wakati wa Afrika kujiweka kama mdau katika uchumi wa kimataifa badala ya kuwa mnufaika wa misaada ya nje pekee.
 
“Afrika haiwezi tena kubaki kama mshiriki asiyekuwa na sauti katika mifumo ya kimataifa ambapo baadhi ya maamuzi muhimu hufanywa bila sauti ya usawa,” alisema.
 
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Mheshimiwa Emmanuel Macron, alisema Bara la Afrika linapiga hatua kubwa za maendeleo na ni bara ambalo halisubiri majawabu ya changamoto bali linatoa majawabu ya changamoto mbalimbali lilazokabiliana nazo.

Katika hatua nyingine, Rais Macron alitangaza uwekezaji wa thamani ya dola za Marekani bilioni 27 barani Afrika katika sekta za nishati, Akili Unde, uchumi wa bahari pamoja na kilimo.
 
“Mpango huu utasaidia kutengeneza takriban ajira 250,000 barani Afrika na nchini Ufaransa,” alisema.
 
Aidha, Rais Macron aliwataka wafanyabiashara wa Afrika kuona fursa zilizopo nchini Ufaransa na kwenda kuwekeza.
 
“Hatuko hapa tu kuja kuwekeza katika Bara la Afrika pamoja nanyi, tunawahitaji viongozi wakubwa wa biashara wa Afrika kuja kuwekeza nchini Ufaransa,” alisema.
 
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema watu wa Bara la Afrika wanapaswa kuwa wa kwanza kunufaika na rasilimali za bara hilo.
 
“Bara hili limebarikiwa rasilimali nyingi, hapa wenyewe ndio wanapaswa wawe wa kwanza kunufaika,” alisema.

Dkt. Mwigulu amemuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *