Rais wa Congo aufungua, ataka Afrika iwanufaishe wananchi wake
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameshiriki Mkutano wa 61 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao umeshirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika na wawakilishi wao ambapo yeye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo ambao umeanza leo (Jumanne, Mei 26, 2026) jijini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo ulifunguliwa na Rais wa nchi hiyo, Denis Sassou-Nguesso na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Makamu wa Rais kutoka nchi mbalimbali.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo ulioanza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kintele (Kintele International Conference Centre), Rais Nguesso alisema Afrika haipaswi kuishia kujivunia kuwa na utajiri wa rasilmali bali izitumie vizuri rasilimali hizo kuwanufaisha wananchi wake.
Alisema ili kuyafikia mageuzi yanayotakiwa, Afrika inahitaji kuwa na miradi ya kimkakati yenye mageuzi. “Tunahitaji kukuza masoko ya fedha na kuziwezesha taasisi za kikanda ili ziweze kukabiliana na vihatarishi vya kiuchumi kupitia ushirikiano imara. Hii itasaidia kuifanya Afrika kuwa na udhibiti wa rasilimali zake na hatimaye kuimarisha uchumi wa nchi pamoja kuboresha maisha wananchi.”
Kaulimbiu ya mwaka huu ya mkutano huo wa 61 inasema: “Kuhamasisha Ufadhili wa Maendeleo ya Afrika kwa Wingi katika Dunia Iliyogawanyika.” (Mobilising Africa’s Development Financing at Scale in a Fragmented World). Kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuziba pengo la kifedha linalokua kwa mahitaji ya maendeleo ya bara la Afrika, hasa katika mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani yanayobadilika kwa kasi.
Baada ya ufunguzi, Waziri Mkuu pia alishiriki mdahalo wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu mustakabali wa ufadhili wa maendeleo barani Afrika (Presidential High-Level Panel on Africa’s Development Financing) ambao uliwashirikisha Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso, Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadéra Rais wa Jamhuri ya Gabon, Brice Clotaire Oligui Nguema na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah.
Katika mdahalo huo, viongozi hao walijadili namna ambavyo nchi za Afrika zinaweza kuimarisha uwezo wa kujitegemea katika kugharamia maendeleo yao kupitia mageuzi ya sekta ya fedha, matumizi ya teknolojia ya kidijitali, ushirikiano wa kikanda pamoja na matumizi bora ya rasilimali za ndani.
Vilevile, Waziri Mkuu alishiriki kwenye mdahalo wa uzinduzi wa taarifa ya African Economic Outlook 2026 na mkutano wa wadau wa maendeleo kuhusu ufadhili wa Mpango wa Uwekezaji wa Blue Fund for the Congo Basin.
Mbali na mikutano hiyo, Waziri Mkuu pia alifanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na taasisi hiyo.
