
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewahakikishia wananchi wa Halmashauri ya Itigi mkoani Singida kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo Barabara ya Mkiwa–Makongolosi ili kuhakikisha inakamilika na kufungua fursa za kiuchumi katika eneo hilo na mikoa jirani.
“Nitakuwa mbunge wa Itigi mpaka hii barabara ikamilike. Barabara hii wala si ya Wanaitigi tu, ni barabara ambayo itafungua shughuli za kiuchumi za kimkoa na hata mikoa jirani,” amesema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu amesema hayo leo Jumapili Mei 31, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Itigi katika Viwanja vya Polisi mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Amesema Serikali imeweka vipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuanza na miradi ambayo wakandarasi wake walikuwa tayari wameanza kazi lakini utekelezaji wake ukapungua kasi, miradi ambayo mikataba yake ilishasainiwa lakini haikuanza kutokana na kutopata malipo ya awali pamoja na miradi ambayo wakandarasi walishapatikana lakini mikataba ilikuwa bado haijasainiwa.
“Tumesema tuanze na miradi ambayo utekelezaji wake ulikuwa umepungua kasi, ile ambayo mikataba ilishasainiwa lakini haikuanza, na ile ambayo wakandarasi walishapatikana ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kabla ya kuanza mingine mipya,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema baadhi ya miradi ilipungua kasi ya utekelezaji kutokana na Serikali kuelekeza nguvu katika kukamilisha miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la Kigongo–Busisi pamoja na miradi mingine ya kimkakati ambayo ilikuwa imekaribia kukamilika.
“Kwa sasa yale mambo yaliyosababisha baadhi ya miradi kupungua kasi tumeyamaliza kwa kiwango kikubwa na tuna uhakika wa kuendelea na utekelezaji wa miradi kwa kasi zaidi,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao ya biashara ikiwemo dengu kwa kuimarisha mifumo ya masoko na kuendelea kufanya mazungumzo na washirika wa biashara ili kulinda maslahi ya wakulima.
“Tunaendelea kufanya mazungumzo na washirika wetu wa biashara ili kuhakikisha wakulima wetu hawapati hasara na mazao yao yanaendelea kupata masoko ya uhakika,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya ardhi na kuwataka viongozi wa serikali za vijiji pamoja na wataalamu wa sekta ya ardhi kusimamia kikamilifu mipango ya matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro inayoweza kusababisha migawanyiko katika jamii.
“Tuendelee kuweka nguvu kubwa kwenye matumizi bora ya ardhi. Ardhi haiongezeki lakini watu wanaongezeka, hivyo lazima tupange matumizi yake kwa busara,” amesema.
Pia ameagiza kusimamiwa kwa karibu matumizi ya fedha za dawa zinazotolewa na Serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki katika vituo vya afya badala ya kuelekezwa kununua dawa katika maduka binafsi.
“Haiwezekani fedha za dawa zipelekwe na Serikali halafu wananchi waambiwe wakazinue dawa mtaani. Hili halikubaliki na lazima lifuatiliwe,” amesema.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amekemea vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma na kuagiza hatua kali kuendelea kuchukuliwa dhidi ya watumishi waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
“Wapo watu waaminifu wengi wa kufanya kazi. Mwizi msimhamishe, akihamishwa anaenda kuiba na huko. Wakamateni na fedha za wananchi zirudi,” amesema.