• Na Mtawala Edison.

    Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Waziri wa Maji kwenda Mkoa wa Mwanza kushughulikia mara moja changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi wa mkoa huo na kuhakikisha huduma hiyo inarejea kwa haraka.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo Jumapili ya Juni 14, 2026, wakati akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Kiomboi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Lulumba, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Amesema amepokea taarifa kuhusu changamoto ya maji katika Mkoa wa Mwanza na tayari amemuelekeza Waziri mwenye dhamana ya maji kwenda eneo husika kusimamia upatikanaji wa suluhisho la haraka.

“Nimemtuma Waziri aende haraka Mwanza akasimamie jambo lile mpaka maji yapatikane. Sisi watu wa Singida tunataka tupate maji toka Mwanza. Simiyu tunataka tupate maji toka Mwanza. Dodoma tunataka tupate maji toka Mwanza. Tabora, wengine wameshaanza kupata maji toka Mwanza. Leo kuja kuambiwa Mwanza, pale pale lilipo Ziwa Victoria, pana shida ya maji. Hili ni jambo ambalo haliwezi kueleweka, na wala hatuwezi kulielewa,” Dkt. Mwigulu.

Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo wakati chanzo cha maji kinajulikana na miundombinu ya mradi ipo.

“Hatutaki ngonjera za maneno. Hawa wanasema si bomba limekuwaje, hawa wanasema si umeme umekuwaje. Chanzo sisi tunajua kiko pale, hatuna shida ya chanzo cha maji, na mradi upo, na maji yapo. Haya mambo mengine ni ya ngonjera, mimi sitaki kuyasikia,”

Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa sekta ya maji pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa haraka.

“Mkuu wa Mkoa awatafute wataalamu wake, awatafute TANESCO na wataalamu wa maji. Wachimbe kiini cha tatizo na wakeshe mpaka wananchi wapate maji. Kunapopambazuka kesho nipate majawabu kwamba maji yamepatikana,”

Juni 9, 2026, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu upungufu wa huduma ya maji uliosababishwa na hitilafu za umeme zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.

MtawalaNews
https://www.instagram.com/p/DZkXsHPgHGE/?igsh=MXM4bWI5eThyMzZ3Mg==

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *