WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kushiriki kugharamia huduma kwa watu wenye ulemavu na watoto walio katika mazingira magumu, akisisitiza kuwa kuwahudumia ni wajibu wa Serikali na jamii.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Jumatatu, Oktoba 5, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, iliyofanyika katika viwanja vya Tanga Beach Resort, jijini Tanga.

“Majukumu yanayohusu watoto wa Kitanzania walioko katika mazingira magumu, watoto wa Kitanzania wenye mahitaji maalum kama hawa, tuyabebe wenyewe kama Watanzania,” amesema.

Ameeleza kuwa kupungua kwa misaada kutoka kwa wahisani wa nje hakujapunguza mahitaji ya makundi hayo, hivyo Watanzania wanapaswa kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa.

Waziri Mkuu amelipongeza kanisa kwa kutoa huduma za elimu, afya na malezi, akisisitiza kuwa watoto hawapaswi kukosa elimu kutokana na ulemavu wa kuona. Pia, amewataka maafisa maendeleo ya jamii kuendelea kuvitambua vituo vinavyohudumia makundi hayo na watu wanaohudumiwa, pamoja na kuhakikisha vituo hivyo vinasajiliwa rasmi ili kurahisisha uratibu wa misaada.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wa halmashauri kuwasaidia watu wenye ulemavu wasioweza kujitegemea badala ya kuwapa barua za kuzunguka kuomba michango.

“Nikasema watu hawa wasiandikiwe barua kwenda kuchangisha, badala yake wachangiwe warudi wakaendeshe maisha yao,” amesema.

Ameeleza kuwa wapo watu wenye ulemavu wanaohitaji mikopo ili kuendeleza shughuli za uzalishaji, huku wengine wakihitaji msaada wa maisha ya kila siku. Amesema ameelekeza wasilazimishwe kujiunga na vikundi ili kupata mikopo na kwamba Serikali inaangalia namna ya kuboresha mifumo ya kuwasaidia wasioweza kujitegemea pamoja na wanaowatunza.

Dkt. Mwigulu amezihakikishia taasisi za dini kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nazo katika utoaji wa huduma za kiroho na kijamii. Amewataka kutumia fursa zinazotokana na marekebisho ya sheria kuhusu hadhi ya taasisi za hisani na misamaha ya kodi, akitaja uwekezaji wa Serikali katika Hospitali ya KCMC na kugharamia mishahara ya watumishi katika baadhi ya taasisi za dini kuwa miongoni mwa mifano ya ushirikiano huo.

Awali, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amesema harambee hiyo inalenga kukusanya Sh. bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha miundombinu, vifaa na mazingira ya utoaji huduma. Ametaja changamoto zinazovikabili vituo hivyo kuwa ni pamoja na uchakavu wa majengo, uhaba wa vifaa vya kisasa, kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na idadi ya watu wanaohitaji huduma.

Ametaja miongoni mwa vituo hivyo kuwa Hospitali za Bumbuli na Kilindi, zahanati nane, Kituo cha Watoto Yatima Irente, Shule ya Msingi ya Wasioona Irente, Kituo cha Watoto wenye Ulemavu wa Akili na Usonji Irente, Korogwe Mental Health Outpatient Clinic na Lutindi Mental Hospital. Amesema vituo hivyo vinahudumia wananchi bila kujali dini, kabila au hali ya kiuchumi.

“Tunapozungumzia maendeleo ya vituo hivi, hatuzungumzii majengo tu; tunazungumzia maisha ya watu, heshima ya mwanadamu, utu, matumaini na mustakabali wa kizazi kijacho,” amesema.

Hadi sasa, harambee hiyo imefikisha Sh. bilioni 1.059, zikiwemo Sh. milioni 617 zilizopokelewa taslimu na ahadi za Sh. milioni 442.

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *