Akemea watoto chini ya miaka mitano kutozwa fedha za matibabu
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema zaidi ya shilingi bilioni 330 zimeingia kwenye Mfuko wa Barabara ndani ya mwezi mmoja baada ya Serikali kuanza kuelekeza fedha moja kwa moja kwenye mfuko huo ili kuharakisha ujenzi na ukarabati wa barabara nchini.
“Sasa hivi tangia tupitishe bajeti, nimeshuhudia ndani ya mwezi mmoja zaidi ya bilioni 330 zimekwenda kwenye mfuko,” alisema Waziri Mkuu leo (Jumamosi, Novemba 7, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika viwanja vya Stendi ya Mwanhuzi, kijiji cha Bomani, wilayani Meatu, mkoani Simiyu.
Alisema Serikali imeweka vipaumbele vitatu katika matumizi ya fedha hizo. Vipaumbele hivyo ni kukarabati barabara muhimu kwa shughuli za kiuchumi, kuwarejesha kazini wakandarasi walioondoka kwa kukosa malipo na kutoa malipo ya awali kwa wakandarasi wanaosubiri kuanza ujenzi.
Akizungumzia huduma za afya, Dkt. Mwigulu alikemea vitendo vya kuwatoza watoto walio chini ya miaka mitano fedha za matibabu. “Miongozo iko wazi, watoto walio chini ya miaka mitano matibabu yake bure. Mnawatoza fedha ya nini?” alihoji.
Aliwataka watumishi wa afya kuwahudumia mara moja wajawazito wanaofika hospitalini wakiwa na uchungu. Pia, alikemea tabia ya kuzitaka familia za wagonjwa wa dharura kuchangisha fedha za mafuta kabla ya kuwapeleka wagonjwa hao kwenye hospitali za rufaa.
Kuhusu barabara ya Nkoma–Lalago yenye urefu wa kilomita 65, Waziri Mkuu alisema mkandarasi atapatiwa malipo ya awali ili aanze ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, alimtaka Waziri wa Ujenzi, Masanja Kungu Kadogosa, kuharakisha usanifu wa barabara inayounganisha Simiyu na Singida kupitia Meatu na Iramba Mashariki ili iingizwe kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Meatu, Salum Khamis Salum, kuhusu uhaba wa maji, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa wilaya washirikiane na wananchi na wataalamu kutathmini pendekezo la kujenga bwawa kwenye Mto Mwanhuzi. Alisema iwapo wataalamu watapendekeza kutumia eneo la bwawa la zamani, viongozi waheshimu uamuzi wa mahakama na wajadiliane kuhusu fidia na wananchi walioshinda kesi.
Kwa upande wa wafugaji, Dkt. Mwigulu alisema Serikali itawalipa fidia wafugaji walioshinda kesi za mifugo na kukuta mifugo yao imekufa walipokwenda kuichukua. Alisema deni la fidia hizo ni takribani shilingi bilioni 3.8.
Awali, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, alisema mji wa Mwanhuzi unahitaji lita milioni 3.8 za maji kwa siku, lakini unazalisha lita milioni 1.7. Alisema maji yamepungua katika Bwawa la Mwanyahina linalohudumia mji huo na visima vitano vilivyochimbwa havikutoa maji ya kutosha kusambazwa kwa wananchi.