
_▪️Dkt. Mwigulu asema elimu ya lazima kuwa miaka 10 kuanzia 2028_
_▪️Asema kila kijiji kitakuwa na sekondari_
_▪️Walimu wa kujitolea watakiwa kutokata tamaa_
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuongeza ajira za walimu nchini kutokana na utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu ya lazima wa miaka 10 unaotarajiwa kuanza mwaka 2028.
Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 16, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kondoa Mjini katika Uwanja wa Puma mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Waziri Mkuu amesema kupitia mfumo huo mpya, Serikali inalenga kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari hatua ambayo itaongeza mahitaji ya walimu, madarasa na maabara nchini.
“Kuanzia mwaka 2028 tunaongelea kila kijiji kitakuwa na sekondari. Maana yake tutahitaji walimu wengi zaidi, maabara zaidi pamoja na madarasa mengi zaidi,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutoa ajira kwa walimu wa masomo mbalimbali hususan sayansi ili kukidhi ongezeko la wanafunzi na utekelezaji wa mitaala mipya.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka walimu wa kujitolea kutokata tamaa kwani Serikali itaendelea kufungua nafasi za ajira kutokana na mahitaji makubwa yatakayojitokeza katika sekta ya elimu.
“Walimu wangu wale ambao mmefanya kazi za kujitolea kwa muda mrefu msikate tamaa, tutaendelea kuhitaji walimu wengi zaidi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema ndani ya siku 100 Serikali iliajiri walimu 7,000 wengi wao wakiwa wa masomo ya sayansi huku akieleza kuwa baadhi ya maeneo bado yana upungufu wa walimu kutokana na ongezeko kubwa la shule za amali na ufundi nchini.
Amesema Serikali pia inaendelea kuandaa wataalamu wa kufundisha masomo ya ufundi ambapo hivi karibuni wanafunzi 150 walipelekwa nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo maalumu yatakayosaidia kukidhi mahitaji ya walimu wa kada hizo.
Mbali na sekta ya elimu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kurejesha kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa imepungua kasi baada ya nguvu kubwa kuelekezwa katika miradi ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, reli ya kisasa ya SGR pamoja na Daraja la Kigongo–Busisi.