Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka, kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

“Utaratibu mzuri wa utawala bora ni ule wa kitaasisi, unaowezesha wananchi kupata haki zao kupitia mifumo imara,” Dkt. Nchemba.

Amesema hayo Jumatano ya Mei 20, 2026 wakati akisikiliza na kushughulikia kero za wananchi wa maeneo ya Mahomanyika, Ndachi, Mbuyuni na Nkuhungu Broad Acres katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Kikao hicho kilihusisha viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu; TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jiji la Dodoma pamoja na wataalamu wa ardhi kutoka ngazi mbalimbali za Serikali.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alipokea taarifa za kina kuhusu hali ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kushughulikia migogoro hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ipo haja ya kufanya mapitio ya kina ya mfumo wa mabaraza ya ardhi kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika upatikanaji wa huduma za mahakama nchini.

Amesema wakati mfumo huo unaanzishwa, lengo lilikuwa kusogeza huduma karibu na wananchi, lakini kwa sasa mahakama zimeenea katika maeneo mengi zaidi hali inayotoa fursa ya kutathmini upya ufanisi wa mfumo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera amesema tayari Serikali imeandaa hati ya mwongozo wa namna ya kushughulikia kesi za ardhi kupitia mahakama na kwamba hatua zilizobaki ni kukamilisha taratibu za uwasilishaji kwa mamlaka husika.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema ongezeko la thamani ya ardhi Jijini Dodoma baada ya Serikali kuhamia Makao Makuu limechangia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi, uvamizi wa maeneo pamoja na biashara holela ya viwanja.

#MtawalaNews
#mtawalaradio
#news
https://www.instagram.com/p/DYkNVisCAPs/?igsh=MTl1dnZ2cThta2VnMQ==

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *