WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana na kujadiliana naye masuala ya kilimo, uvuvi na uchumi wa bluu.

Mazungumzo hayo yalifanyika jana (Jumanne, Oktoba 20, 2026) kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue) ulioanza Oktoba 20, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, Marekani.

Katika majadiliano yao, Waziri Mkuu alimshukuru Dkt. Mukeshimana kwa ufadhili unaotolewa na IFAD kwenye uvuvi wa bahari kuu chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na uendelezaji wa uchumi wa bluu kupitia Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi ya Zanzibar.

“Hii miradi ni ya muhimu na inapewa kipaumbele zaidi kwani inasaidia kuzalisha ajira kwa wanawake na vijana,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa IFAD, Dkt. Mukeshimana aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa kitovu cha upatikanaji wa chakula kwa maeneo yanayoizunguka. “Binafsi ninawapongeza kwa sababu mmeendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula cha uhakika barani Afrika. Mnafanya kazi kubwa na nzuri mno ya kulisha chakula kwenye maeneo ya jirani,” alisema.

Kipekee, Dkt. Mukeshimana alimsifu Dkt. Mwigulu akisema: “Tanzania imebahatika sana kupata Waziri Mkuu ambaye zamani alishawahi kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye akawa Waziri wa Fedha. Siyo kila nchi imepata bahati kama hiyo, Tanzania mmebarikiwa sana.”

Alisema taasisi hiyo itaendelea kufadhili miradi inayolenga kuondoa njaa na umaskini kwa kuwekeza kwa watu wa vijijini, kuwezesha ushiriki wao katika masoko na kuimarisha ustahimilivu wa hali ya hewa wa maisha yao.

Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.

Share Story

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *