
Ahimiza kuunganisha usafiri wa majini na njia nyingine za usafirishaji_
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi inayounganisha nchi hizo moja kwa moja ili kupunguza muda wa kusafirisha mizigo na kuwawezesha wananchi kufikia masoko kwa urahisi.
“Afrika ni moja na njia za kuiunganisha Afrika zilizo rahisi na za asili bila kuwa watumwa wa mipaka ni kutengeneza miundombinu itakayorahisisha shughuli za wananchi za kiuchumi kufanyika kwa urahisi zaidi; hiyo ni njia ya kawaida ya asili isiyo na mikutano mingi na yenye vitendo vingi,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 15, 2026) wakati akifungua mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Shirika la Wanamaji la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (Maritime Organisation for Eastern, Southern and Northern Africa – MOESNA) uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwigulu amesema ukosefu wa miundombinu inayounganisha nchi moja kwa moja unasababisha mizigo inayosafirishwa ndani ya Afrika kuchukua muda mrefu kuliko inayotoka mabara mengine.
“Huu utaratibu wa mzigo kutoka bara lingine kufika Afrika kwa haraka kuliko mzigo wa hapa hapa utamalizwa tu kama tutatengeneza hii miundombinu ya aina hii,” amesema na kuongeza:
“Ninaambiwa Uganda walikuwa wanapeleka maziwa Afrika ya Magharibi lakini yale maziwa yamechukua miezi miwili na nusu karibu miezi mitatu na huenda maziwa kutoka bara lingine yangeweza kuwahi kufika.”
“Hivyo, hata usafiri mwingine wowote kama ambavyo kwenye mjadala wenu mmesema, lazima uendane na usafiri wa majini kwani nyakati nyingine kwenda nchi mojawapo ya Afrika inabidi uende Ulaya ndipo urudi kwa jirani yako. Hiyo na yenyewe haiwezi ikawafikisha wananchi wa Afrika kwenye masoko yao,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha usafiri wa majini na njia nyingine za uchukuzi, akisema hali ya baadhi ya safari kati ya nchi za Afrika kulazimika kupitia Ulaya inazuia wananchi kufikia masoko yao kwa urahisi.
Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema Tanzania imepata heshima kubwa ya kushiriki uenyekiti wa MOESNA na kwamba ina dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchukuzi wa majini.
“Tunaamini kuwa maendeleo ya sekta hii ni msingi muhimu wa kukuza biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira, na kuimarisha uchumi wa nchi zetu. Tutaweka msisitizo katika kuimarisha usafirishaji wa majini, kuongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, kuendeleza wataalamu, na kukuza uchumi wa buluu,” alisema.
Alisema Tanzania inataka kuona MOESNA inakuwa chombo cha kuleta matokeo halisi ya kiuchumi badala ya kuwa jukwaa la mikutano na maazimio pekee.